Thursday, September 21, 2017
Home > CCM > Taarifa Ya Umoja Wa Vijana Wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Iliyotolewa Leo Juni 30,2017 Upanga, Dar es salaam.

Taarifa Ya Umoja Wa Vijana Wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Iliyotolewa Leo Juni 30,2017 Upanga, Dar es salaam.

  VMM/C.10/41Vol.II/9   30/06/2017
TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI IJUMAA JUNI 30, 2017.

Itakumbukwa kuwa kuanzia mwezi wa April, 2017 Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake kilianza mchakato wa kutoa Fomu za kugombea nafasi mbali mbali kwa wanachama wake kwa kipindi cha 2017 – 2022.

Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM inawashukuru na kuwapongeza Vijana wote waliojitokeza kuomba Nafasi mbali mbali ndani ya Chama na Jumuiya wakitimiza matakwa ya Katiba ya CCM Ibara ya 13 kifungu (a) na (c) ya Kanuni ya Umoja wa Vijana wa CCM kwa hakika wametimiza haki na wajibu wao wa Kidemokrasia.

Kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchukuaji wa Fomu ngazi ya Tawi na Kata/Wadi na sasa kuelekea katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya1977 toleo la 2012 Ibara ya 14(3) na Kanuni ya UVCCM Ibara ya 80 kifungu (e) Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM anawajulisha na kuwatangazia Vijana wote wa Chama Cha Mapinduzi wenye sifa za Kikanuni na Kikatiba kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kushika nyadhifa mbali mbali za Uongozi katika Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania.

Nafasi ambao zitagombewa ni:-
(i)Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa.
(ii)Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa
(iii)Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Nafasi 3 Tanzania Bara na Nafasi 2 Zanzibar.
(iv)Wajumbe wa Baraza Kuu Viti (5) vya Taifa; Nafasi 3 Tanzania Bara na Nafasi 2 Zanzibar.
(v) Mjumbe 1 wa kuwakilisha UVCCM katika Jumuiya ya Wazazi
(vi)Mjumbe 1 kuwakilisha UVCCM katika Jumuiya ya Wanawake (UWT)
(vii) Wajumbe wa Baraza Kuu 5 wanaowakilisha Vyuo na Vyuo Vikuu Nafasi 3 Tanzania Bara na Nafasi 2 Zanzibar.

Fomu za kugombea Nafasi hizo zitatolewa kuanzia tarehe2 – 10 Julai, 2017 katika Ofisi ya UVCCM, Makao Makuu Dodoma ghorofa ya 3 chumba Na. 45  Ofisi ya UVCCM Upanga, Dar es Salaam ghorofa ya 7 na Ofisi Ndogo ya UVCCM Gymkana Zanzibar kuanzia Saa 2.00 Asubuhi hadi Saa 10.00 Jioni bila ya malipo ya aina yoyote.

Ofisi ya Katibu Mkuu inawakumbusha wale wote watakaojitokeza kuchukua Fomu za kugombea Nafasi mbali mbali baada ya kukamilisha mchakato wa kujaza na kurejesha wanatakiwa kutulia na kuendelea na majukumu yao mengine na taratibu zinazofuata watajulishwa baadaye kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.

Ni mwiko na marufuku kwa mtu yeyote kuzunguka, kupitapita kwa njia yoyote kuonesha dalili za kushawishi makundi ya watu au kupita kusema nafasi aliyoomba kwa watu au katika Vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii hatutasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za UVCCM, Maadili na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa mawasiliano maulizo, ama jambo lolote la msaada wa ki muongozo unaweza kuwasiliana kwa simu 0754 926 601,
0653 384 235, 0625 137 881.

Tunawatakia kila la heri na maandalizi mema.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Jokate Urban Mwegelo

Kny: KATIBU MKUU



Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *