Thursday, September 21, 2017
Home > Featured_Slider > Anza Ya Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Dkt Magufuli Kwa Kampuni Ya IPTL Yatimia.

Anza Ya Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Dkt Magufuli Kwa Kampuni Ya IPTL Yatimia.

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imekataa kuiongezea muda wa leseni Kampuni ya kufua umeme wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL) baada ya leseni yake ya kuzalisha umeme kumalizika muda wake.

Agosti 30 mwaka huu kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA ilisema kuwa kikao chake kilichofanyika kimefikia uamuzi wa kutiongezea kampuni hiyo leseni ya biashara.

Machi 28 mwaka huu, IPTL iliwasilisha maombi EWURA ikiomba kuongezewa muda wa leseni yake ya kufanyakazi nchini kwa miezi 55 kuanzia Julai 16, 2017 hadi 15 Januari 2022.

Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA imesema kuwa imezingatia mambo mbalimbali katika kuikatalia IPTL maombi yake ambayo ni, athari hasi kwenye bei ya umeme kwa watumiaji endapo muda wa leseni ya IPTL ungeongezwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kulipa malipo ya ‘capacity charge’ kwa kiasi cha dola 2.667 milioni kwa mwezi.

Sababu nyingine iliyotajwa na EWURA ni mapingamizi yaliyowasilishwa kutoka kwa umma na wadau mbalimbali kufuatia kutakiwa kutoa maoni yao kuhusu ombi la IPTL la kuongezewa muda wa leseni ya biashara. IPTL pia ilikataa kutokana na mashtaka yanayoihusu kampuni hiyo ambayo bado yapo mahakamani.

Kampuni ya IPTL ambayo inahusishwa na kashfa ya uchotwaji mabilioni ya fedha kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow ilikuwa na mkataba wa miaka 20 ambao ulimalizika Julai 16, mwaka huu, na kwa miaka yote hiyo imekuwa ikiiuzia umeme serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia mitambo hiyo ya kufua umeme iliyoko eneo la Salasala Tegeta jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli mara kadhaa amekuwa akisikika akisema kwamba anataka Tanzania iwe na umeme wa uhakika ili kuweza kufikia uchumi wa viwanda lakini pia waachane na umeme wa matepeli ambao wamekuwa wakiibia serikali, ambapo alikuwa akiilenga kampuni ya IPTL.

Akiweka jiwe la msingi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II, Rais Magufulialisema,“Ni lazima nchi yetu tuachane na umeme usio na uhakika, umeme wa kukodishakodisha, umeme wa kutumia watu na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi mara IPTL, mara nini, ni kwa sababu tulizoea maumeme ya kukodisha kodisha ya wafanyabiashara, kwa hiyo hatua hii ya umeme wetu, ambao tutaumiliki sisi wenyewe tutafanikiwa katika maendeleo.”
“Tuachane na mitambo ya kukodi, tumechoka kufanyishwa biashara na wawekezaji, tunalipia `capacity charge’ za ajabu ajabu halafu tunalipia bei ya ajabu.”

Wabia wa IPTL, Harbinder Singh wa Kampuni ya PAP na James Rugemalira wa VIP Engineering Limited wako mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi pamoja na kutakatisha fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *