Thursday, September 21, 2017
Home > Featured_Slider > Shaka Ateta Na Wabunge Vijana Mjini Dodoma.

Shaka Ateta Na Wabunge Vijana Mjini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka amefanya kikao kazi na wabunge wanaowakilisha vijana wa Chama Cha Mapinduzi katika Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi Mjini Dodoma.

Shaka alisema kuwa Uwepo wa wabunge vijana katika Bunge la 11 ni jambo jema kwani wabunge hao wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi wametumia vizuri nafasi zao kama wawakilishi kuwasemea vijana ili kuwa chachu ya kuwasaidia vijana nchini kutambua fursa zilizopo na namna bora ya kuondokana na umasikini.

Aliwapongeza wabunge hao vijana na kusema kuwa wao ni hazina ya Taifa, uwepo wao katika chombo hicho cha kutunga sheria, utakuwa wenye tija zaidi kwa kuhakikisha haijitokezi mihemko inayoweza kugeuza mantiki ya chombo hicho.

Alisifu wabunge hao kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Bunge tangu siku ya kwanza kwa maslahi makubwa ya Taifa wamekuwa wachangiaji wazuri wa mijadala kwa kutumia lugha zenye staha ndani ya Bunge.

Shaka alisema uwepo wa wabunge hao vijana umekuwa chachu bungeni huku akisema kuwa maelekzo ya semina elekezi kwa wabunge hao vijana wameyazingatia vyema kwani wamekuwa na heshima, nidhamu na uadilifu katika kuzungumza na kufikisha ujumbe ili bunge liendelee kuwa na hadhi yake kwa wananchi.

Aidha Shaka amesisitiza zaidi wabunge hao kutambua kuwa uwakilishi wao unatokana na vijana nchini hivyo wanapaswa kutumia vyema nafasi zao Bungeni kuibua chachu ya hamasa ya maendeleo kwa vijana kwa kutoa mbinu mbadala kwa viajana ili kuwainua kifikra katika muktadha wa kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Wabunge hao walimpongeza Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuimarisha umoja huo kupitia mikutano mbalimbali aliyoifanya katika ziara zake katika mikoa ya Tanzania na wamemuhakikishia kumpa ushirikiano zaidi ili kuendelea kutekeleza vyema majukumu yake.

Hata hivyo Wabunge walipongeza kikao hicho muhimu na kumuhakikishia kuwa kwa kuwa ubunge wao unatokana na CCM hivyo wataendelea kuisimamia na kutekeleza majukumu yao ya kibunge lakini zaidi majukumu ya chama kwani ndio msingi wa Uongozi wao.

Katika Bunge la 11 Chama cha Mapinduzi CCM kinawakilishwa na wabunge vijana 6 ambao ni Mhe Maria Kangoye, Mhe Zainab Katimba, Mhe Khadija Nassir Ally, Mhe Halima Abdallah Bulembo, Mariam Ditopile na Mhe Munira Mustapha Khatib.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *